Psalms 52

Hukumu Ya Mungu

Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi amekwenda nyumbani kwa Ahimeleki.”

1 aEwe jitu, mbona unajivunia ubaya?
Kwa nini unajivuna mchana kutwa,
wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?
2 bUlimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi.
Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.
3 cUnapenda mabaya kuliko mema,
uongo kuliko kusema kweli.
4 dUnapenda kila neno lenye kudhuru,
ewe ulimi wenye hila!

5 eHakika Mungu atakushusha chini
kwa maangamizi ya milele:
atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu
kutoka hema yako,
atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai.
6 fWenye haki wataona na kuogopa,
watamcheka, wakisema,
7 g“Huyu ni yule mtu ambaye
hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,
bali alitumainia wingi wa utajiri wake,
na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”

Neema Ya Mungu

8 hLakini mimi ni kama mti wa mzeituni
unaostawi katika nyumba ya Mungu,
nautegemea upendo wa Mungu usiokoma
milele na milele.
9 iNitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,
nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.
Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.
Copyright information for SwhNEN